Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamemkamata mshukiwa wa ulanguzi wa watoto katika kaunti ya Trans Nzoia.
Operesheni hiyo iliyotekelezwa katika eneo la Kiminini, ilifanikisha kuokolewa kwa mtoto huku maafisa hao wakipata stakabadhi za kutiliwa shaka kutoka kwa mshukiwa huyo.
Kulingana na DCI kwenye ukurasa wake wa X, mshukiwa huyo Gilbert Nyabuto mwenye umri wa miaka 56, alifumaniwa katika kijiji cha Nyamira akiwa na mvulana wa umri wa miaka 10 baada ya wananchi kushuku mienendo yake.
“Mshukiwa huyo alijitambulisha kama Naibu Kamishna wa Idara ya Ujasusi Nchini (NIS) na kutoa kitambulisho kilichoashiria cheo hicho pamoja na nambari ya huduma,” ilisema DCI.
Hata hivyo baada ya upekuzi zaidi, mshukiwa huyo alipatikana na stakabadhi za watu tofauti pamoja na barua bandia ya kujiunga na Vikosi vya Ulinzi (KDF), na hivyo kuibua wasiwasi kuhusu shughuli zake.
DCI ilisema alipohojiwa, mshukiwa huyo alidai kuwa alikuwa akimsaidia mtoto huyo kupata nyumba, huku wote wawili wakipelekwa katika kituo cha polisi cha Kiminini kwa uchunguzi zaidi.
Mtoto huyo tayari ameunganishwa na familia yake katika eneo la Salona, naye mshukiwa anaendelea kuzuiliwa uchuguzi ukiendelea kubainisha shughuli zake.