Maafisa wakuu watatu wa sekta ya nishati leo Jumamosi wamejiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa ya uagizaji mafuta ya ubora wa kiwango cha chini hapa nchini.
Maafisa hao ni pamoja na Katibu wa Idara ya Petroli Mohamed Liban, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Kenya Pipeline Jose Sang na Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) Daniel Kiptoo Bargoria.
Kujiuzulu kwa maafisa hao kumethibitishwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix koskei, kupitia kwa taarifa leo Jumamosi.
Maafisa hao walijiuzulu baada ya kukamatwa na Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI kuhusiana na madai ya kuingiza hapa nchini mafuta ya ubora wa viwango vya chini na hivyo kukiuka taratibu za uagizaji mafuta zilizopo.
Kulingana na Koskei, uchunguzi wa awali unaashiria kuwa maafisa waliojukumiwa na usimamizi wa usambazaji bidhaa za petroli, wamevuruga data ya hifadhi ya mafuta kuashiria kuwa kuna upungufu wa mafuta hapa nchini.
“Rais amesikitika kuwa wale waliojukumiwa kusimamia mfumo wa usambazaji mafuta, wamevuruga data kuhusu kiwango cha mafuta kinachohifadhiwa. Hatua hii huenda ilitekelezwa kutokana na ongezeko la mafuta duniani, na hivyo kubuni dhana potovu kuna upungufu wa mafuta,” alisema Koskei kwenye taarifa hiyo.
Koskei aliongeza kuwa uagizaji huo wa mafuta haukuzingatia mfumo wa ununuzi kati ya serikali na serikali (G2G), ulioanzishwa mwaka 2023.