Polisi wanasa kilo 255 za bangi ya thamani ya shilingi milioni 7.6 Kilifi

Dismas Otuke
1 Min Read

Maafisa wa polisi wamenasa bangi ya kilo 255 katika kaunti ya Kilifi na kumtia mbaroni mwanamke wa umri wa miaka 29 anayeshukiwa kuendesha biashara ya ulanguzi wa mihadarati.

Polisi kutoka kitengo cha kukabiliana na mihadarati kutoka kituo cha Malindi, wakishirikiana na wenzao kutoka kituo cha Watamu,waliendesha msako  katika nyumba ya mshukiwa  kijijini Jimba baada ya kupewa vidokezo na umma.

Mwanamke huyo aliye na umri wa miaka 29 kwa jina Winfred Nkatha, alipatikana na magunia manane yaliyosheheni misokoto ya bangi iliyokaushwa ndani ya chumba chake.

Bangi hiyo ya uzani wa kilo 255 inakisiwa kuwa ya thamani ya shilingi milioni 7.65.

Mshukiwa baadaye alipelekwa katika kituo cha Watamu ambako amezuiliwa akisubiri kufikishwa kortini.

Share This Article