Miano: Sekta ya utalii ilikusanya shilingi bilioni 500 mwaka 2025

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano.

Wizara ya Utalii na Wanyamapori imesema idadi ya watalii waliozuru maeneo tofauti hapa nchini mwaka 2025, iliongezeka hadi watalii milioni 7.9

Kwenye ripoti iliyotolewa na wizara hiyo,  watalii milioni 2.7 walikuwa wa kutoka mataifa ya nje, huku watalii milioni 5.2 wakiwa wa nyumbani.

Akitangaza ripoti hiyo, Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano,  alisema katika kipindi hicho, wizara hiyo pia  ilikusanya shilingi bilioni 500, hiki kikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kunakiliwa.

Miano alisema idadi ya watalii kutoka nje iliongezeka kwa asilimia 9, ishara kwamba Kenya inasalia kuwa chaguo bora kwa shughuli za kitalii.

Waziri huyo alidokeza kuwa utalii wa nyumbani unaendelea kuwa nguzo kuu, inayokinga sekta ya utalii dhidi ya misukosuko kutoka nje.

“Marekani inasalia kuwa soko kubwa la utalii hapa nchini, huku tukiendelea kupanua wigo wetu kufikia masoko ibuka kama vile India na China,” alisema Miano.

Alisema ufanisi katika sekta hiyo ya Utalii umetokana na kuimarishwa kwa mifumo ya uunganishaji na ushirikiano thabiti kati ya wadau.

Share This Article