Mike Sonko aondokea biashara ya pombe

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko ametangaza kwamba ameondokea biashara ya pombe kabisa, ikizingatiwa kwamba alichagua kuacha kutumia pombe na kusonga karibu na Mungu.

Alikuwa akizungumza alipozuru eneo lake la burudani la Volume VIP Club, ambalo alielezea kwamba alilifunga na hataki kurejelea biashara hiyo hata ingawa bado ana shehena ya pombe humo.

“Tangu nilipochagua kuacha pombe na kumkaribia Mungu, nimeamua kuacha pia biashara ya pombe kabisa,” aliandika Sonko kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Kuhusu hatima ya eneo hilo la burudani Sonko alisema, “Nitauza au kukodisha klabu cha usiku cha Volume VIP Club, au nipeane pombe yote. Huu ni ukurasa mpya katika maisha yangu.”

Katika siku za hivi karibuni, Sonko ameonekana kubadilisha pakubwa mitindo yake ya maisha ambapo anaonekana pia kupoteza uzani wa mwili kwa kiwango kikubwa.

Inaripotiwa kwamba alishauriwa na madaktari akabadilisha mitindo ya maisha ambapo sasa amekumbatia mazoezi ya mwili, kuhakikisha anapata lishe bora na analala vyema.

Mabadiliko hayo yanaonyesha mwelekeo mpya kutoka kwa mtindo wa maisha wa kifahari uliomtambulisha hadharani awali, ambao ulijumuisha kuonekana mara kwa mara katika kumbi za burudani za usiku na ushiriki katika miradi ya burudani.

Volume VIP Club ni moja kati ya biashara za Sonko katika sekta ya ukarimu na burudani.

Klabu hiyo ya usiku ilianzishwa baada yake kuondolewa madarakani kama gavana wa Nairobi mwaka 2020, alipogeukia biashara binafsi na ujasiriamali wa burudani za usiku, hasa katika eneo la pwani.

Share This Article