Mwimbaji wa nyimbo za injili wa Rwanda Alexis Dusabe ataandaa tamasha nchini Ubelgiji mwezi ujao na itakuwa mara yake ya kwanza kabisa kufanya hivyo.
Hafla hiyo itakayofanyika Mei, 5, 2026 huko Rue Birmingham 54 itatumiwa kusherehekea miaka 25 ya uimbaji wa nyimbo za injili kwa Dusabe.
Haya yanajiri miezi mitatu tu baada yake kuandaa hafla sawia jijini Kigali nchini Rwanda. Ameipa hafla hiyo jina la wimbo “Umuyoboro” ambao alitoa miaka 25 iliyopita wakati akianza kazi kama mwimbaji.
Awali kulikuwa na hali ya sintofahamu baada ya mratibu wa awali, Team Productions, kuripotiwa kujiondoa katika kuandaa tukio hilo.
Hali hii ilifuatia tangazo la tamasha tofauti la wasanii wa injili Ben na Chance, lililopangwa kufanyika katika BK Arena tarehe 5 Aprili.
Mratibu alipendekeza kuahirisha tamasha la Dusabe ili kuepuka mgongano wa ratiba, lakini mwimbaji huyo aliamua kuendelea peke yake kwa kushirikiana na timu yake iliyoko Ubelgiji.
Tangu kuanzisha kazi yake mwaka 2000, Dusabe ameendelea kuwa msanii thabiti na mwenye ushawishi mkubwa katika muziki wa injili, akitoa nyimbo nyingi ambazo zimemuweka miongoni mwa wasanii wakuu wa kizazi chake.
Tamasha la Brussels litakuwa onyesho lake la kwanza nje ya Rwanda—hatua muhimu katika safari yake ya miaka 25. Tracy Agasaro na Rene Patrick pia wanatarajiwa kutumbuiza.
Wakati huo huo, Ben na Chance wamekuwa wakiongeza juhudi katika mazoezi kuelekea tamasha lao la Easter Jubilee katika BK Arena. Wasanii wengine wanaotarajiwa kushiriki katika tukio hilo ni pamoja na Papy Clever, Dorcas, na wawili chipukizi wa injili Alicia na Germaine.
Baada ya tamasha la Pasaka, wanapanga kurejea Ulaya (Ubelgiji, Ujerumani, Uingereza) na baadaye kutumbuiza Amerika Kaskazini.