Rais Ruto kusaidia wasanii kulinda kazi zao kisheria

Rais alikutana na baadhi ya wasanii wa Gengetone na Urbantone katika ikulu ya Nairobi leo.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ameahidi usaidizi wa kisheria kwa wasanii fulani wa mtindo wa Gengetone na wa Urbantone waliofanya mkutano naye katika Ikulu ya Nairobi leo.

Katika taarifa, kiongozi wa nchi alifichua kwamba wasanii husika walimwelezea kuhusu madhila wanayokumbana nayo katika kazi zao kama wabunifu huku akiahidi usaidizi.

Rais alitaja kunyakuliwa kwa nyimbo nyingi za wasanii hao kutokana na mizozo ya hakimiliki baada yao kuingia kwenye mikataba na kampuni za kimataifa.

Kulingana na Rais, wasanii walioathiriwa kwa jumla wamepoteza umiliki wa nyimbo zaidi ya 700, ukiwemo wimbo maarufu uitwao “Sipangwingwi” ulioimbwa na Exray.

Rais alitaja hali hiyo kuwa ya kusikitisha, akibainisha kuwa wabunifu wachanga wanaendelea kunyanyaswa licha ya mchango wao mkubwa katika utambulisho wa kitamaduni wa Kenya na tasnia ya burudani.

Ili kushughulikia suala hilo, Ruto alisema amerahisisha upatikanaji wa msaada wa kisheria ili kuhakikisha wasanii wanawakilishwa ipasavyo mahakamani wanapojaribu kurejesha haki zao.

Aliongeza kuwa serikali inashirikiana na wadau mbalimbali kuweka hatua za vitendo zinazolenga kulinda maslahi ya wanamuziki na kuhakikisha wanapata malipo ya haki kwa kazi zao.

Mkuu wa Nchi alifichua pia kwamba ameelekeza Bunge la Kitaifa, kupitia kwa Kiongozi wa Wengi, kuharakisha mchakato wa Mswada wa Uchumi wa Ubunifu wa mwaka 2026 pamoja na mageuzi muhimu ya hakimiliki.

Sheria hiyo inatarajiwa kuimarisha ulinzi wa mali ya ubunifu na kutoa mfumo salama zaidi kwa sekta ya ubunifu inayokua nchini.

Aidha, Ruto alitangaza kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali kwenye jukwaa la serikali la e-Citizen ili kurahisisha ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha.

Mpango huo unalenga kuongeza uwazi na kuhakikisha wasanii wanapata mapato yao kwa wakati na kwa usawa kutokana na kazi zao.

Hatua ya Rais inajiri wakati ambapo kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu udhaifu wa wasanii wa Kenya katika soko la kidijitali la kimataifa.

Hata hivyo ukosefu wa ulinzi wa kutosha wa kisheria na mikataba isiyo ya haki imewaacha wengi bila udhibiti wa kazi zao wenyewe.

Share This Article