Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amepata kibali cha kukamatwa kwa afisa wa uhamiaji anayehudumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya afisa huyo kukosa kukfika mahakamani kukiri mashtaka.
Kibali hicho kimetolewa na Jaji Gideon Kiage na kesi dhidi ya mshukiwa imeratibiwa kusikilizwa Aprili 8 mwaka huu.
John Poriot alipaswa kufikishwa mbele ya mahakama ya Kahawa na kushtakiwa chini ya ya Sheria Kupambana na Ulanguzi wa Watu, Namba. 8 ya mwaka 2010.
Anatuhumiwa kwa kuwezesha Wakenya wawili kuondoka nchini kinyume cha sheria kwa dhamira ya kutafuta fedha. Inadaiwa kuwa Oktoba 3 mwaka 2024 katika uwanja wa JKIA katika kaunti ndogo ya Embakasi, afisa huyo kwa pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani, waliwalangua Evans Kipyegon na Isaac Kipruto kwa kuwalaghai kuwa wangepata ajira nchini Thailand.
Mshtakiwa pia anakabiliwa na shtaka la pili la kuwa na shilingi 11,087 anazoshukiwa kupata kwa njia ya kihalifu.