Baraza la Magavana lamtetea Sakaja

Martin Mwanje
2 Min Read
Mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi akiwahutubia wanahabari

Baraza la Magavana (CoG) limemtetea vikali Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja na kutoa wito wa kuondolewa kwa agizo la kukamatwa kwake. 

Agizo hilo lilitolewa na Kamati ya Uhasibu wa Umma (CPAC) baada ya Sakaja kukosa kufika mbele yake mara nne.

Akiwahutubia wanahabari leo Jumanne, mwenyekiti wa CoG ambaye pia ni Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi pia ameonya dhidi ya matumizi ya nguvu dhidi ya Magavana wanaokosa kufika mbele ya CPAC.

Mivutano imeibuka kati ya Magavana na Maseneta huku Maseneta wakilimbikiziwa madai ya utapeli na wakuu hao wa kaunti.

Ni madai ambayo Maseneta wamepuuzilia mbali wakisema hiyo ni njama ya Magavana kukwepa uwajibikaji.

Awali kwenye taarifa, Gavana Sakaja alipuuzilia mbali agizo lililotolewa na Bunge la Seneti kwa Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja la kutaka akamatwe.

Alidai kuwa hatua ya kutofika mbele ya kamati ya Bunge la Seneti ilitokana na mwongozo wa Baraza la Magavana, lililowashauri kutofika mbele ya CPAC hadi masuala yaliyoibuliwa na baraza hilo yatakapotatuliwa.

“Swala lililopo sio la kibinafsi kuhusu Gavana Sakaja, lakini ni swala linaloshughulikiwa kwa pamoja na Baraza la Magavana,” alisema Sakaja kwenye taarifa hiyo.

Aliongeza kuwa mzozo kati ya Magavana na Maseneta unapaswa kusuluhishwa kitaasisi na wala sio kwa kumlenga Gavana binafsi.

Wakati huo huo, Sakaja ambaye pia ni Seneta wa zamani wa Nairobi alidokeza kuwa awali alifika katika kamati kadhaa za Seneti ikiwa ni pamoja na ile kuhusu Ardhi na Mazingira juma lililopita.

Alishutumu jinsi maafisa wa polisi walivyotumwa kumkamata, akihoji uhalali wa operesheni hiyo.

“Hakuna haja ya kuzua kizaazaa wakati wa usiku.”

Mnamo siku ya Jumatatu usiku, maafisa wa polisi walizingira afisi za serikali ya kaunti ya Nairobi zilizoko katikati mwa jiji la Nairobi wakitaka  kumkamata Sakaja.

Hatua hiyo ilifuatia agizo la Seneti lililomwagiza Inspekta Mkuu wa Polisi kumwasilisha Gavana huyo mbele ya kamati ya Seneti.

Sakaja anahitajika kujibu maswali ya ukaguzi wa matumizi ya fedha ya kaunti hiyo mwaka 2024/25.

Share This Article