Taarifa ya Joseph Mwanjala
Seneta wa kaunti ya Bungoma David Wafula Wakoli ameelezea wasiwasi kuhusu zaidi ya vitambulisho vya kitaifa 100,000 ambavyo havijachukuliwa katika kaunti ya Bungoma.
Wakoli alikuwa akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea afisi za IEBC kaunti ya Bungoma kukagua jinsi zoezi jipya la usajili wa wapiga kura lililoanza jana Jumatatu linavyoendelea.
Ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani, chini ya uongozi wa Kamishna wa kaunti ya Bungoma Thomas Sankei, pamoja na wasimamizi na viongozi wa eneo hilo, kushirikiana katika kutambua na kusambaza vitambulisho hivyo.
Wakoli alisema ni muhimu kwamba wamiliki halali wachukue vitambulisho vyao ili waweze kutumia haki zao za kidemokrasia kwa kujiandikisha kama wapiga kura na kushiriki katika kuwachagua viongozi mnamo mwaka 2027.
Seneta huyo amewapongeza vijana wote wanaojitokeza kwa wingi kujiandikisha kama wapiga kura na kuwataka waliosalia kuendelea kuandikisha.
Kulingana na Grace Rono, mratibu wa IEBC katika kaunti ya Bungoma, wana vifaa 162 vya usajili vilivyosambazwa katika maeneo bunge 9, na vifaa vya ziada vinapatikana katika taasisi za masomo katika kaunti nzima.
Rono alisema kwamba baadhi ya vifaa pia vitawekwa katika ofisi za IEBC na vituo vya Huduma Centre.