Miili yote 33 iliyozikwa katika kaburi la pamoja huko Kericho ilitoka katika Hospitali ya Rufaa ya Nyamira.
Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI Mohamed Amin amesema hili lilibainika wazi kufuatia uchunguzi uliofanywa na maafisa wa idara hiyo.
Shughuli ya ufukuaji wa miili kwenye kaburi hilo iliongozwa na maafisa wa DCI.
Ufukuaji huo ukibaini kuwa miili 33 ilizikwa kwenye kaburi hilo, 25 ikiwa ya watoto na 8 ya watu wazima.
Maafisa hao wamekuwa wakifanya uchunguzi wa ilikotoka miili hiyo.
Uchunguzi wao ukibaini kuwa miili hiyo ilisafirishwa kutoka Hopitali ya Rufaa ya Nyamira baada ya kukosa kuchukuliwa kwa muda mrefu kutoka chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
Awali, Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo alidai ni miili 13 pekee iliyotoka katika kaunti yake, madai ambayo yanakinzana na uchunguzi wa DCI.
Watu wawili walikamatwa kuhusiana na sakata hiyo. Wao ni afisa wa Afya ya Umma wa kaunti ya Nyamira na mlinzi wa makaburi ya umma ambako miili hiyo ilizikwa.
Wawili hao wamekuwa wakiwasaidia maafisa wa polisi katika uchunguzi.
Taarifa hii imechangiwa na mwanahabari wetu Erick Kiplangat