Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, imetoa orodha ya miili 480 ambayo haijachukuliwa na inaendelea kuhifadhiwa kwenye makafani yake.
Kupitia ilani kwa umma leo Jumanne, hospitali hiyo ilisema kati ya miili hiyo 480, miili 102 ni ya watu wazima huku miili 378 ikiwa ya watoto.
Ilitoa wito kwa familia kufika kwenye makafani hayo na kutambua miili ya wapendwa wao ndani ya siku saba, ikionya kuwa itatafuta idhini ya mahakama ya kuizika iwapo haitachukuliwa ndani ya muda huo, kuambatana na sheria za Afya ya Umma.
“Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta inahifadhi miili ambayo haijachukuliwa na wenyewe. kuambatana na sheria ya Afya ya Umma sehemu ya 224 ya mwaka 1991, wananchi wanahimizwa kutambua miili ya wapendwa wao na kuichukua ndani ya siku saba, ila sivyo hospitali hiyo itatafuta idhini ya mahakama kuizika,’ ilisema sehemu ya ilani hiyo.
kulingana na sheria ya Aya ya Umma ya mwaka 1991, mwili haupaswi kuhifadhiwa kwa mafakani ya umma kwa zaidi ya siku 10.
Aidha miili ambayo haijachukuliwa kwa siku 21, inaweza zikwa na hospitali husika au mamlaka ya eneo hilo kwa mujibu wa sheria.