Takriban watu 66 wamefariki baada ya ndege ya Jeshi la Anga la Colombia iliyokuwa imebeba watu 128 kuanguka Jumatatu katika eneo la Puerto Leguízamo, mkoa wa Putumayo, kusini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Peru.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Anga, Carlos Fernando Silva Rueda, kulikuwa na watu 128 wakiwemo wanajeshi, na wafanyakazi ndani ya ndege aina ya C-130 Hercules wakati wa ajali hiyo.
Vyanzo vya habari vinasema kuwa watu wasiopungua 66 wamefariki, huku watu wanne wakiwa hawajulikani walipo, idadi iliyothibitishwa pia na vyanzo viwili vya kijeshi. Gavana wa mkoa wa Putumayo, Jhon Gabriel Molina, naye alithibitisha idadi hiyo.
Hata hivyo, wakati mamlaka zikisubiri takwimu rasmi, chanzo cha jeshi kililiambia BBC Mundo kuwa ripoti ya hivi karibuni inaonyesha vifo vinaweza kufikia 44, na huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Kabla ya kutolewa kwa takwimu hizo mpya, Rais wa Colombia, Gustavo Petro, alisema kuwa wanajeshi vijana 83 walikuwa bado hai wakati huo.
Waziri wa Ulinzi, Pedro Sánchez, alisema ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa, ikidondoka takriban kilomita 1.5 kutoka uwanja wa ndege ilikotoka.
Aliongeza kuwa watu kadhaa waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, na kwamba taarifa kamili kuhusu waliojeruhiwa na waliopoteza maisha itatolewa mara tu itakapothibitishwa rasmi.
Awali, waziri huyo alithibitisha kuwa taratibu zote za kuwasaidia waathiriwa na familia zao zimeanzishwa, pamoja na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.
Taarifa ya BBC