Wanachama saba wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi, NLC wamekula kiapo cha utenda kazi katika hafla iliyoandaliwa leo Jumatatu asubuhi katika majengo ya mahakama.
Hafla hiyo iliongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome ambaye pia ni Rais wa Mahakama ya Juu.

Walioapishwa ni mwenyekiti mpya wa NLC Dkt. Abdillahi Saggaf Alawy na wanachama Susan Khakasa Oyatsi, Daniel Murithi Muriungi na Kigen Vincent Cheruiyot.
Wengine ni Dkt. Julie Ouma Oseko, Mohamed Abdi Haji Mohamed na Seneta mteule wa zamani Mary Yiane Seneta.
Wote hao wamekula kiapo baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu kwenye tume hiyo kwa kipindi cha miaka sita.
Awali, walipigwa msasa na bunge na uteuzi wao kuidhinishwa.
Kwenye hotuba yake, Jaji Koome amewataka kutumikia taifa kwa uadilifu na kuangazia madhila yaliyozagaa katika sekta ya ardhi.