Timu za Misri, Pyramids FC na Al Ahly, zilikiona cha mtema kuni baada ya kubanduliwa katika kipute cha Ligi ya Mabingwa Afrika ziliposhindwa nyumbani Jumamosi.
Pyramids walivuliwa ubingwa baada ya kulemewa mabao 2-1 na FAR Rabat ya Morocco kwenye marudio ya robo fainali na kusalimisha taji kwa kipigo cha jumla ya magoli 3-2 kufuatia sare ya 1-1 katika duru ya kwanza wiki jana.
Mabingwa mara 12 Al Alhy nao wakiwa nyumbani Cairo waligutushwa baada ya kucharazwa mabao 3-2 na Esperance ya Tunisia.
Esperance, waliokuwa wamepata ushindi wa goli moja bila jibu katika mkumbo wa kwanza wa kwota fainali wiki jana, walifuzu kwa nusu fainali kwa ushindi wa jumla ya magoli 4-2.