Viongozi wa kidini walalamikia ukosefu wa usalama Meru

Maeneo kadhaa ya kaunti ya Meru yamekuwa yakikumbwa na ujambazi na wizi wa mifugo.

Marion Bosire
2 Min Read

Viongozi wa kidini katika kaunti ya Meru wamejiunga na wenzao wa kisiasa katika kupaaza sauti kuhusu hali inayoendelea kushuhudiwa ya ukosefu wa usalama.

Wimbi la ukosefu wa usalama limekumba maeneo ya malisho ya kaskazini mwa Kaunti ya Meru, ambapo maisha yamepotea na mifugo kuibwa katika matukio ya mara kwa mara ya ujambazi na wizi wa mifugo.

Viongozi hao wa kidini wanatoa wito kwa serikali ya kitaifa kuchukua hatua madhubuti kurejesha usalama katika eneo hilo.

Wakiongozwa na Askofu Kiogora Magambo wa Kanisa la House of Praise, ambaye pia analenga wadhifa wa ugavana wa Meru mwaka 2027, viongozi hao wa kidini walielezea hali hiyo kuwa ya kusikitisha.

Walibainisha kuwa watoto wengi wameachwa bila wazazi na wanawake wengi wamekuwa wajane kufuatia mashambulizi ya kikatili ya majambazi wenye silaha.

Kauli za viongozi wa Kikristo zimeungwa mkono na wenzao wa Kiislamu kutoka Laare na Mutuati katika eneo la Igembe Kaskazini, Kaunti ya Meru.

Eneo hilo ni moja kati ya maeneo yaliyoathirika zaidi na ukosefu wa usalama kutokana na ujambazi na wizi wa mifugo.

Waislamu hao wakiongozwa na Sheikh Adam Osman pia waliwataka wanasiasa kote nchini kujiepusha na lugha ya uchochezi na matusi, wakionya kuwa kauli kama hizo zinaweza kudhoofisha zaidi amani na mshikamano.

Mohammed Omar, ambaye pia ni kiongozi wa Kiislamu kutoka Laare, aliitaka Wizara ya Usalama wa Ndani kuchukua hatua za haraka kurejesha usalama Tigania na Igembe, ambapo ujambazi na wizi wa mifugo bado ni changamoto kubwa.

Viongozi wa Kiislamu walibainisha kuwa mashambulizi ya mara kwa mara yamesababisha vifo vya watu wengi na kuacha familia nyingi katika umaskini baada ya kupoteza mifugo wao.

Waliongeza kuwa ukosefu wa usalama unaoendelea pia umeathiri elimu, huku watoto wengi wakishindwa kuhudhuria shule kwa kuhofia usalama wao.

Share This Article