Viongozi wa nchi za Kenya na Uganda William Ruto na Yoweri Museveni wamesifia mradi wa upanuzi wa reli ya kisasa waliozindua kwa pamoja.
Uzinduzi huo ulifanyika hyko Kibos katika kaunti ya Kisumu, siku moja tu baada ya Rais Ruto kutekeleza uzinduzi sawia katika kaunti ya Narok.
Katika hotuba yake kwenye hafla hiyo huko Kisumu, Rais Ruto alisema kwamba wakati umewadia wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika kila sehemu ya nchi.
Aliwasuta wanaoingiza siasa katika ajenda yake ya mabadiliko akisema anashirikiana na wakenya wengine wenye maono sawa katika kufanikisha maendeleo kote nchini na hatakwazwa na yeyote.
Rais Museveni kwa upande wake alisema kwamba reli hiyo ya kisasa itapunguza pakubwa gharama ya kufanya biashara.
Kulingana naye, mizigo mizito itasafirishwa kupitia reli hiyo tofauti na hali ya sasa ambapo inasafirishwa kupitia barabara hali inayoharibu barabara.
Aliongeza kuwa ajali pia zitapungua huku gharama ya usafirishaji nayo ikipungua.
Museveni alizitaka nchi za kanda ya Afrika Mashariki kuanzisha asasi za kifedha zinazoendeshwa na serikali ili kusaidia kutoa mikopo nafuu kwa wawekezaji.