Kesi ya uchaguzi wa Mbeere Kaskazini kusikilizwa mwisho leo Alhamisi

Vikao vya kusikiliza kesi hiyo vilianza Machi 9, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Vikao vya kusikiliza kesi inayopinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa eneo la Mbeere Kaskazini vinatarajiwa kufikia kikomo leo Alhamisi.

Shughuli hiyo iliyoanza Jumatatu, Machi 9, 2026 mbele ya Jaji Richard Mwongo wa Mahakama Kuu ya Embu, iliingia siku ya nane na ya mwisho hii leo.

Idara ya mahakama imekuwa ikipeperusha mubashara matukio ya kesi hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Kesi mbili ziliwasilishwa mahakamani kupinga uchaguzi wa Leo Wamuthende kama mbunge wa Mbeere Kaskazini kwenye uchaguzi mdogo ulioandaliwa kufuatia hatua ya Rais ya kumteua aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Geoffrey Ruku kuwa Waziri.

Jaji Mwongo hata hivyo alitupilia mbali keshi ya kwanza kutokana na hatua ya wawasilishaji kukosa kufuata maagizo ya idara ya mahakama ya kutoa ada ya shilingi laki 8.

Kesi ya pili iliyowasilishwa na Newton Kariuki almaarufu Newton Karish aliyewania wadhifa huo kwenye uchaguzi huo mdogo, ilikubaliwa na mahakama kuu na ndiyo vikao vyake vinatarajiwa kukamilika leo, kusubiri hukumu.

Karish wa chama cha DP anapinga matokeo ya uchaguzi huo akisema ulikumbwa na kasoro kadhaa ikiwemo utambuzi wa aliyeibuka mshindi.

Kulingana naye, Wamuthende alitumia majina tofauti wakati wa mchakato wa uteuzi na katika karatasi za kura na kwamba hakuwa mpiga kura aliyesajiliwa kwa kutumia jina alilotumia kwenye uchaguzi.

Karish anasema kwamba alipobadilisha jina kisheria kutoka Leonard Muriuki Njeru hadi Leo wa Muthende, mabadiliko hayo hayakufanywa kwenye sajili ya wapiga kura ya IEBC.

Jingine analodai Karish ni kwamba kulikuwa na udanganyifu wakati wa kupiga kura, uhongaji wa wapiga kura na utambuzi wenye dosari.

Mwisho wa vikao hivyo leo, Jaji Mwongo anatarajiwa kutoa tarehe ambayo atasoma hukumu yake.

Share This Article