Mwanamume wa umri wa miaka 23 amehukumiwa kifungo cha miaka 45 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya mauaji.
Mahakama Kuu ya Kisumu ilimpata Arnold Ochieng Omollo na makosa ya kumuua kaka yake mdogo na mpwa wake.
Alihukumiwa kifungo hicho baada ya yeye mwenyewe kukiri kutekeleza mauaji hayo, licha ya kufahamishwa adhabu ya kosa hilo.
Mahakama ilifahamishwa kuwa kati ya Novemba 24 na 25, 2024, Omollo alitekeleza mauaji ya wawili hao wakiwa na umri wa chini ya miaka 10 walipokuwa wamelala kwa kutumia silaha hatari.
Ni mauaji yaliyotekelezwa katika kijiji cha Kamango, kaunti ndogo ya Nyakach, kaunti ya Kisumu.
Uchunguzi wa miili ulibainisha kuwa wawili hao walifariki kutokana na majeraha ya kichwani yaliyopenyeza hadi kwenye ubongo.
Kiongozi wa mashtaka Mercy Muema alifahamisha mahakama kuwa, mshtakiwa alimuua Aaron Smith Omollo (nduguye) na Jayson Havi (mpwa wake), wote wenye umri mdogo na ambao hawakuwa na uwezo wa kujikinga, huku akitaka mahakama kumpa adhabu kali.
Ikitoa hukumu hiyo, mahakama ilisema upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha, zikiwemo silaha zilizotumika kwenye mauaji hayo.