Wakazi wa eneo la Mundika, Busia wahofia usalama wao

radiotaifa
2 Min Read

Taarifa ya Sayyid Abdalla

Wakazi wa eneo la Mundika viungani mwa mji wa Busia wanahofia usalama wao baada ya mhudumu wa duka la Mpesa kuuawa na majambazi katika duka lake sokoni Mundika jana Jumatatu alasiri.

Yamkini mwendazake mwenye umri wa miaka 25 alipigwa risasi na majambazi hao nje ya duka hilo saa saba mchana, kabla ya majambazi hao kufyatua risasi kiholela kuwafurusha wafanyabiashara na wananchi kwenye soko hilo na kutoweka na pesa taslimu shilingi elfu mia nane.

Majambazi hao wawili waliojihami na bunduki aina ya AK 47 na pikipiki isiyokuwa na nambari ya usajili walitowekea kwenye barabara ya Busia-Adungosi ikiaminika waliingia taifa jirani la Uganda kupitia njia za mkato.

Wananchi na viongozi waliojawa na hamaki wamekashifu vikali kisa hicho cha kusikitisha wakiwasuta vikali maafisa wa usalama kwa kuzembea kazini na kupelekea visa vya mauaji na wizi kushamiri katika eneo hilo la Mundika.

Mwakilishi wadi ya Bukhayo Magharibi Peter Taalam anasema kuwa inasikitisha kuona mhudumu wa Mpesa anavamiwa na kuuliwa wakati Rais William Ruto alipokuwa maeneo ya Nasewa kilomita 4 kutoka eneo la tukio kwenye ziara yake ya Magharibi, akitilia shaka mikakati ya usalama eneo hilo.

Aidha, wenyeji wa Mundika wamesisitiza kuwa maafisa wa polisi wa kambi za Esikulu na Mabatini Korinda wanapaswa kupewa uhamisho wa lazima kwani usalama umedorora pakubwa katika siku za hivi karibuni.

Share This Article