Spika Wetang’ula ataka sheria ya trafiki kupitiwa upya

Wito wake unawadia siku chache baada ya ajali kutokea eneo la Malaha, Webuye na kusababisha vifo vya watu 16 na wengine wapatao 20 kujeruhiwa.

Martin Mwanje
2 Min Read
Spika Moses Wetang'ula wakati wa ibada ya watu 16 waliofariki eneo la Malaha, Webuye.

Kuna haja ya kupitia upya sheria ya trafiki ili kuchukua hatua kali dhidi ya madereva wazembe ambao ni chanzo cha ajali za barabarani zinazoshuhudiwa nchini mara kwa mara.

Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula wakati wa ibada ya watu 16 waliofariki katika ajali eneo la Malaha kwenye barabara ya Webuye-Kitale Machi 9.

Watu wengine wapatao 20 walipata majeraha na wanaendelea kupokea matibabu hospitalini.

Ibada hiyo iliandaliwa katika bewa la Webuye la Chuo Kikuu cha Masinde Muliro leo Jumatatu.

Wetang’ula amelalamika kuwa familia nyingi zinaendelea kupoteza wapendwa wao kupitia ajali barabarani, jambo analosema linapaswa kukomeshwa mara moja.

Alisema sheria ya trafiki inapaswa kufanyiwa marekebisho ili kuwachukulia hatua madereva wazembe ambao nyakati zingine hutoroka punde baada ya kusababisha ajali.

Amedokeza kuwa tayari amejadili pendekezo hilo na kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na kumtaka kuharakisha marekebisho hayo ili kukabiliana na jinamizi la ajali barabarani.

Ajali iliyotokea katika eneo la Malaha ilidaiwa kusababishwa na dereva wa lori la masafa marefu ambaye alipoteza mwelekeo na kugonga magari kadhaa pamoja na wapita njia.

Majeruhi walipelekwa katika hospitali ya kaunti ya Webuye kwa matibabu huku miili ya  waliofariki  ikipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo punde baada ya kutokea kwa ajali.

Wito unazidi kutolewa kwa madereva kuwa waangalifu ili kuepuka kusababisha ajali ambazo matokeo yake huwa ni mauti katika maeneo mbalimbali nchini.

Share This Article