Mwanamuziki wa Uganda Ivan Bugembe Ssentamu maarufu kama Dax Vibez amefichua kwamba hatua ya kakake mkubwa Bobi Wine ya kukaa mbali na familia imesaidia kuimarisha usalama wao.
Dax Vibez ambaye ni kaka mdogo wa Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, alikuwa akizungumza kwenye mahojiano.
Alikiri kwamba amekua katika maisha kwa kufuata maelekezo ya Bobi Wine na ndugu zake wengine.
Hata hivyo msanii huyo analalamika kwamba safari ya kisiasa ya Bobi Wine imeathiri sana familia kwani sasa kila mwanafamilia ni mlengwa wa maadui zake.
Vibez sasa anahisi kwamba, uamuzi wa Bobi Wine wa kukaa mbali na familia unapunguza hatari kwa wanafamilia.
“Wakati anakaa mbali na sisi, tunakuwa salama kwa kiwango fulani. Kuwa kwake karibu nasi huleta ukosefu wa usalama. Tunaishi kwa woga na sasa tuko salama kwa sababu yuko mbali,” alisema Vibez.
Hata ingawa wana wasiwasi kuhusu usalama wao, Dax Vibez alisema familia inajivunia safari ya kisiasa ya Bobi Wine na anavyopigania uongozi wa nchi ya Uganda.
Bobi Wine, ambaye ni Rais wa chama cha kisiasa cha National Unity Platform – NUP, alitangaza kwa njia ya video kwamba ameondoka Uganda na kutafuta makazi salama ughaibuni.
Wine alijitokeza na kutoa ujumbe huo baada ya zaidi ya miezi miwili tangu uchaguzi ulipoandaliwa nchini Uganda.
Amekuwa akisisitiza kwamba alishinda uchaguzi huo lakini Rais Museveni akapendelewa.