Rais Ruto awakabidhi funguo wamiliki wapya wa nyumba Emgwen

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto amewakabidhi funguo wamiliki wapya wa nyumba Emgwen.

Rais William Samoei Ruto siku ya Alhamisi amekabidhi nyumba za mpango wa Boma Yangu kwa wamiliki wapya katika mtaa wa Emgwen, kaunti ya Nandi.

Wakati wa hafla hiyo, wamiliki wapya 120 walipokea funguo za nyumba zao, huku kiongozi wa taifa akisema mpango wa  ujenzi wa nyumba za gharama nafuu umefanikisha ukuaji wa maeneo bunge 111 kupitia utoaji wa makazi bora kwa wananchi pamoja na kubuniwa kwa fursa za ajira kwa vijana na wanawake.

“Baadhi ya watu walisema hatutajenga, wengine walisema nyumba hizo zitakabidhiwa watu mashuhuri, lakini tazama, wanaonufaika ni watu wa hapa na wafanyabiashara,” alisema Rais Ruto.

Kati ya wakazi hao 120 waliopokea nyumba hizo, watano kati yao wanaishi na ulemavu.

Paul Koech Limo ambaye mguu wake mmoja uliumia kwenye ajali ya barabarani mwaka 2009, anasema alijisajili kwenye mpango wa Boma Yangu mwaka 2023 na alianza kuwekeza mwaka 2024. Sasa anamiliki nyumba yenye vyumba viwili vya kulala.

Wakati wa ziara yake katika kaunti ya Nandi, Rais Ruto aliweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika mradi wa Chesumei, huku akielezea kujitolea kwa serikali kujenga nyumba za garama nafuu katika kaunti hiyo hatua itakayobuni nafasi za ajira kwa wakazi wa eneo hilo.

Share This Article