Taarifa ya Bruno Mutunga
Vikundi vya wanawake kutoka maeneo ya uhifadhi wa mazingira katika kaunti ya Isiolo vimeanza kupokea majiko ya kisasa yanayookoa nishati.
Hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi ya kuni na makaa huku ikiboresha afya za familia na kulinda mazingira.
Majiko hayo mapya hutumia kiwango kidogo cha kuni au makaa, hupika haraka na kutoa moshi kidogo, hali inayosaidia kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba ambao huathiri zaidi wanawake na watoto wadogo wanaokaa muda mrefu karibu na maeneo ya kupikia wakati wa maandalizi ya chakula.

Wataalamu kutoka shirika la “Climate and Clean Air Coalition” wanasema kuwa kati ya watu bilioni 2.1 hadi 2.5 duniani bado wanatumia moto wa wazi au majiko yanayotumia kuni, mabaki ya mimea na makaa. Matumizi haya yanachangia pakubwa uchafuzi wa hewa majumbani unaosababisha takribani vifo milioni 3.2 vya mapema kila mwaka, huku wanawake na watoto wakiathiriwa zaidi.
Usambazaji wa majiko hayo unaendeshwa kupitia Mpango wa Mashinani Works kwa ushirikiano na Northern Rangelands Trust, kwa ufadhili kutoka Ubalozi wa Denmark nchini Kenya.
Mpango huo unalenga kuwafikia zaidi ya wanawake 500 kutoka jamii za hifadhi za mazingira katika kaunti ya Isiolo, ambao wengi wao hutegemea kuni na makaa kwa shughuli za kupika kila siku. Kwa kutumia majiko hayo mapya, wanufaikaji wanatarajiwa kupunguza matumizi ya mafuta, kupunguza gharama za kupika na kutumia muda mfupi kuandaa chakula.
Washirika wa mradi wanasema mpango huo pia utachangia katika uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti katika maeneo ya malisho ya Isiolo ambayo ni nyeti na ambayo uoto wake umeendelea kupungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
Saadia Mohamed, mmoja wa wanufaikaji wa mradi huo, aliukaribisha mpango huo akisema utasaidia kuboresha afya na kulinda mazingira katika kaunti hiyo.
Alisema matumizi ya majiko yanayookoa nishati yatapunguza kwa kiasi kikubwa athari za moshi ambao mara nyingi husababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa wanawake na watoto katika familia nyingi.
“Familia nyingi hapa hutegemea makaa na kuni kupika, jambo linalozalisha moshi mwingi ndani ya nyumba zetu. Majiko haya mapya yatasaidia kupunguza magonjwa yanayotokana na moshi na pia kulinda mazingira yetu,” alisema.
Afisa wa Mpango wa Moto Safi Mashinani, Ture Boru, alisema mradi huo umebuniwa kuwawezesha wanawake katika maeneo ya vijijini na mijini ambao bado wanategemea sana mbinu za jadi za kupika.
Alieleza kuwa majiko hayo mapya hayapunguzi tu matumizi ya kuni na makaa bali pia hupunguza muda wa kupika, hivyo kuwapa wanawake nafasi ya kushiriki katika shughuli zingine za kujipatia kipato pamoja na majukumu ya familia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Waziri anayesimamia Idara ya Mazingira, Maji, Nishati na Maliasili katika kaunti ya Isiolo Guracha Kikuyu Sarite, alisema mpango huo umewadia kwa wakati mwafaka kwani unaendana na juhudi za kaunti za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kulinda mazingira.
Afisa huyo wa kaunti alieleza matumaini yake kuwa mradi huo utaboresha maisha ya wananchi huku ukisaidia juhudi pana za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kulinda maliasili katika eneo hilo.