Maafisa wa polisi jijini Entebbe nchini Uganda wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa cha kutoweka kwa kocha mkongwe wa soka nchini humo.
Kocha Mike Hillary Mutebi anaripotiwa kutoweka Machi 7, 2026.
Katika taarifa kwenye mtandao wa X, polisi wa Uganda hususan wa kituo cha polisi cha Entebbe walielezea kwamba wanachunguza kisa cha Mutebi ambaye alikosa kurejea nyumbani baada ya kuhudhuria semina katika ufuo wa Kisubi.
Taarifa ya polisi pia ilielezea kwamba semina aliyohudhuria Mutebi siku hiyo ilikuwa imeandaliwa na kanisa Katoliki na alionekana kwa mara ya mwisho saa 12 unusu jioni, wakati waliohudhuria semina hiyo walikuwa wakijiaandaa kurejea jijini Kampala.
“Mutebi alihudhuria semina ya kanisa Katoliki katika ufuo na alionekana mara ya mwisho saa 12 unusu wahudhuriaji walipokuwa wakijianda kusafiri kurejea Kampala,” walisema polisi katika taarifa.
Waliongeza kwamba walipowasili Kawempe, Mutebi hakuwepo na hakuna aliyefahamu alikokwenda.
Wametoa wito kwa umma kusaidia maafisa wa polisi na habari zinazoweza kusaidia kumpata kocha huyo. Habari hizo zinaweza kuwasilishwa kwa kituo chochote cha polisi au kupitia nambari ya simu 0775318345.
Waandalizi wa tuzo za soka nchini Uganda ndio walitoa tangazo kuhusu kutoweka kwa kocha Mutebi wakisema walipokea habari hizo kutoka kwa familia yake.
Kulingana na familia hiyo, simu za Mutebi zimezimwa tangu wakati waligundua kwamba ametoweka.