Mwanamuziki wa kike nchini Nigeria Tiwatope Omolara Savage, maarufu kama Tiwa Savage, amezindua rasmi wakfu wake.
Nyota huyo wa mtindo wa muziki wa Afrobeats alizindua “Tiwa Savage Music Foundation” katika hafla iliyohudhuriwa na watu maarufu katika tasnia ya burudani nchini Nigeria, katika eneo la Delborough, jijini Lagos jana.
Akihutubia waliohudhuria hafla hiyo, Savage wa umri wa miaka 46 alielezea kwamba lengo kuu la wakfu huo ni kuboresha ujuzi katika sehemu mbali mbali za tasnia ya muziki, zaidi ua utumbuizaji tu.
“Wakfu huu utashughulikia kila kitu kinachohusu muziki, uundaji filamu, utangazaji wa kazi za muziki, muziki wa kuliwaza, utayarishaji na uhandisi wa sauti.” Savage alisema.
Taasisi hiyo itapunguza pia pengo kati ya walio na talanta na upatikanaji wa mafunzo ya kitaalamu na fursa za ughaibuni.
Mwimbaji huyo alikiri kwamba Nigeria ina talanta nyingi, na anachotaka kufanya ni kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu hitajika, elimu na anaweza pia kuwa daraja la kuwafikisha katika rubaa tofauti wanamuziki wanaoibuka.
Wabunifu 100 watachaguliwa na wakfu huo na watahudhuria mafunzo ya kina ya siku nne Aprili 23 hadi 26 mwaka huu jijini Lagos.
Chuo cha muziki cha Berklee ambacho Savage alisomea kinahusika pakubwa katika utoaji wa mafunzo hayo.
Wanamuziki, watayarishaji muziki, waandishi wa nyimbo na wabunifu wengine wamehimizwa kutuma maombi ya nafasi hizo 100 za kwanza.