Hazina ya kitaifa ya miundombinu yazinduliwa

Rais William Ruto alisema hazina hiyo mpya itasaidia Kenya kufadhili miradi muhimu ya miundombinu na kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ametia saini kuwa sheria mswada wa Hazina ya Kitaifa wa Miundombinu, na hivyo kuzindua hazina ya kitaifa ya miundombinu. 

Hatua hiyo kulingana na kiongozi wa nchi, inaashiria mabadiliko makubwa katika mkakati wa maendeleo wa nchi.

Akizungumza leo Machi 9, 2026, rais alisema hazina hiyo mpya itasaidia Kenya kufadhili miradi muhimu ya miundombinu huku ikipunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje.

Sheria hiyo inaweka mfumo wa kukusanya akiba za ndani ya nchi, hasa fedha za hazina ya pensheni, ili kusaidia uwekezaji wa muda mrefu katika barabara, reli, bandari, makazi, nishati na unyunyiziaji mashamba maji.

Kulingana na rais, Kenya inahitaji takriban dola bilioni 4 kila mwaka ili kukidhi mahitaji yake ya miundombinu, huku Afrika ikikabiliwa na pengo la ufadhili linalokadiriwa kufikia dola bilioni 80 kila mwaka.

Ruto alisema hazina hiyo imechochewa na ajenda ya mageuzi ya kiuchumi ya Bottom-Up ya serikali, inayolenga kupanua fursa za kiuchumi na kuhakikisha haki za kikatiba kama makazi, huduma za afya na elimu zinatimizwa kwa vitendo.

Mradi wa kwanza mkubwa utakaofadhiliwa kupitia mfumo huu mpya utakuwa upanuzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Mradi huo unatarajiwa kupata takriban shilingi bilioni 20 kama mtaji kutoka kwa mfuko huo na wawekezaji wa taasisi za ndani.

Mtaji wa kwanza wa hazina hiyo utatokana na mpango wa kuorodhesha kampuni ya serikali ya Kenya Pipeline katika soko la hisa la Nairobi, hatua iliyokusanya shilingi bilioni 106.

Serikali inatarajia kuongeza thamani ya kiasi hicho hadi mara kumi na mbili na hivyo kukusanya hadi shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Ruto alisema mpango huo unaashiria mwanzo wa sura mpya katika ufadhili wa maendeleo ya Kenya kwa kutumia mtaji wa ndani kujenga maendeleo ya taifa.

Share This Article