Mwanamuziki wa Marekani Stefani Joanne Angelina Germanotta, maarufu kama Lady Gaga huenda akafunga ndoa na mpenzi wake Michael Polansky hivi karibuni.
Gaga aliashiria ujio wa ndoa hiyo katika kipindi cha mitandaoni cha Bruno Mars kiitwacho ‘Romantic Radio’ kwa ushirikiano na iHeartRadio, kupitia ujumbe wake ulionakiliwa.
Bruno aliuliza kuhusu yajayo ambapo sauti ya Lady Gaga inasikika ikimjibu kwamba yeye na mpenzi wake wamekuwa wakisafiri mwaka mzima lakini wanaoana hivi karibuni.
“Mimi na mpenzi wangu tumekuwa tukisafiri mwaka mzima, lakini tunaoana karibuni. Tunatumai kwamba utatuchagulia wimbo spesheli kwa ajili yetu.” alisema Gaga.
Bruno hakuzumgumzia suala la wawili hao kufunga ndoa hivi karibuni na badala yake aliamua kufurahikia ombi la Gaga. Alimchagulia Gaga na Polansky kibao chake kiitwacho “Risk It All” kutoka kwa albamu yake mpya.
Mazungumzo ya hivi punde kuhusu ndoa ya Lady Gaga na Polansky yanajiri miezi kadhaa baada ya mwanamuziki huyo kufichua kwamba walikuwa wanafikiria kuhusu kufunga ndoa.
Novemba mwaka jana, Polansky aliambia jarida la Rolling Stone kwamba wangependelea harusi ya faragha ya watu wao wa karibu pekee badala ya hafla ya kufana na kijionyesha.
Mwaka 2024 alipoonekana kwenye kipindi cha Jimmy Kimmel Live, Gaga alisema Polansky alikuwa amemchumbia kwenye chumba cha hoteli waliporejea kutoka ziara ya kukwea mlima.
Polansky alipiga goti alipokuwa akimchumbia na akamvisha pete siku hiyo. Gaga alitangaza uchumba wao kwa mara ya kwanza kwenye michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka 2024.