Mutua afafanua kuhusu mwonekano wa Mary Atieno

Marion Bosire
2 Min Read
Ezekiel Mutua, Mkurugenzi Mtendaji MCSK

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hakimiliki za Muziki nchini, MCSK Dkt. Ezekiel Mutua ametoa taarifa kuhusu picha iliyosambaa mitandaoni ya mwimbaji wa nyimbo za injili Mary Atieno.

Katika taarifa hiyo, Mutua alielezea kwamba picha hiyo ilipigwa wakati wa kesha kanisani na kamwe haiashirii hali ya sasa ya mwimbaji huyo.

Aliendelea kumtetea Atieno akisema anaohudhuria kesha mara nyingi huwa hawajinadhifishi sana.

Huku akikubaliana na wanamitandao kwamba Mary Atieno anahitaji usaidizi wa serikali, wahisani, mashabiki na Wakenya, Mutua alisisitiza haja ya utoaji wa taarifa sahihi.

Mutua alifichua pia kwamba marafiki na mashabiki wa mwimbaji huyo wakiongozwa na Larry Liza, hivi maajuzi walimzawadi Mama Mary Atieno nyumba mpya mtaani Buruburu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alichapisha picha kadhaa za hafla ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Mary Atieno wakati alikabidhiwa funguo za nyumba hiyo.

Anachohitaji Mary kwa sasa kulingana na Mutua ni fanicha ili kumwezesha kuishi maisha mema wakati huu ambapo umri wake umekwenda huku akikaribisha michango.

Mary Atieno alizaliwa bila uwezo wa kuona lakini alifanikiwa kupata elimu hadi chuo kikuu na amekuwa akihudumu kama mwalimu katika shule ya upili ya wasichana ya Buruburu.

Hivi maajuzi picha yake ilisambaa mitandaoni ikimwonyesha akiwa na mavazi ambayo wengi walionelea kwamba sio ya hadhi yake na kutaka asaidiwe.

Share This Article