Taarifa ya BBC
Kampuni ya nishati inayomilikiwa na serikali ya Qatar, QatarEnergy, inasema imesitisha uzalishaji wa gesi asilia ya kimiminika (LNG) baada ya mashambulizi ya Iran kwenye baadhi ya vituo vyake.
Inasema vituo vilivyoshambuliwa vilikuwa Ras Laffan – kituo cha usindikaji wa gesi cha ufukweni – na Mesaieed – eneo jingine muhimu kwa uzalishaji wa gesi asilia wa Qatar.
Taifa hilo la Ghuba ni mojawapo ya wazalishaji wakuu wa gesi asilia ya kimiminika duniani, pamoja na Marekani, Australia na Urusi.
Bei ya gesi yapanda kwa kasi katika masoko ya kimataifa
Bei ya gesi imepanda sana katika masoko ya kimataifa kutokana na mvutano uliopo Mashariki ya Kati.
Nchini Uingereza muda mfupi baada ya saa sita mchana, gesi asilia iliyokuwa inawasilishwa kwa ajili ya mwezi Aprili ilikuwa ikiuzwa kwa 42%, kwa zaidi ya 112p kwa kila nishati ya joto.
Qatar ni muuzaji mkuu wa gesi asilia iliyoyeyushwa, ikichangia takriban moja ya tano ya usambazaji wa gesi duniani – na nyingi ya gesi hii husafirishwa kwa njia ya bahari kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Ingawa wateja wakuu wa Qatar wako Kusini na Mashariki mwa Asia, usumbufu wowote wa biashara hiyo unaweza kusababisha ongezeko la bei katika masoko ya kimataifa, kwa sababu huongeza ushindani wa usafirishaji kutoka kwingineko.
Hali hiyo imezidishwa na kufungwa kwa baadhi ya vituo vya kuzalisha gesi nchini Israeli kama tahadhari ya usalama.
Wachambuzi wanasema hili linaweza kuwa tatizo kubwa kwa Ulaya, kwani ingawa majira ya baridi kali yanakaribia kuisha na matumizi yanapungua, akiba ya gesi katika eneo hilo inapungua na itahitaji kujazwa tena wakati wa kiangazi.