Mwanamuziki tajika wa asili ya Congo Antoine Christophe Agbepa Mumba maarufu kama Koffi Olomide amehalalisha ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu Candy Nkunku ambaye wengi wanamfahamu kama Cindy Le Coeur.
Wawili hao Koffi wa umri wa miaka 69 na Cindy wa umri wa miaka 43, walifanya harusi ya kiserikali iliyohudhuriwa na watu wao wa karibu pekee.
Koffi alitoa tangazo hilo kwa umma jana kwa kuchapisha video fupi inayomwonyesha yeye na Cindy kwenye hafla hiyo wakati wimbo wao wa taifa ulikuwa ukipigwa.
Mwanamuziki huyo aliandika, “Furaha yetu na iwe yenu”.
Leo Jumatatu Machi 2, 2026, Koffi kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii alichapisha video nyingine fupi inayomwonyesha akitoa ahadi zake kwa Cindy huku umati ukishangilia.
Chini ya video hiyo ameandika, “Ninawaombea kwamba katika furaha yetu ni mwangwi wa furaha yenu na mshiriki nasi furaha yetu. Hamjambo na Jumatatu yenye furaha kwenu”.
Kando na kawaida ya harusi ambapo bibi harusi huvaa mavazi ya rangi nyeupe, Cindy aliamua kuvaa vazi la rangi ya dhahabu, lilipambwa kwa maua ya rangi ya waridi.
Koffi naye alikuwa amevaa koti ya kung’aa ya rangi ya dhahabu na suruali ya rangi nyeupe.
Nyota huyo wa muziki toka Congo alikuwa kwenye ndoa awali na Aliane Olomide aliyemwoa mwaka 1993 na kutalikiana naye mwaka 2023 na ana watoto watano.
Uhusiano wa kimapenzi kati ya Koffi na Cindy umekuwepo muda mrefu na wamekuwa hata wakishirikiana naye katika kazi ya muziki kwenye bendi ya Koffi iitwayo Quartier Latin.
Wakati mmoja mwaka 2023, Cindy alijipata akishambuliwa katika mitandao ya kijamii kufuatia kile ambacho wengi walikitaja kuwa kuharibu ndoa ya Koffi na kuwa na ushindani na binti ya Koffi aitwaye Didi Stone.
Watu maarufu, wnamuziki wenza na hata masgabiki wamekuwa wakipongeza waili hao kwa hatua waliyopiga.