Iran yathibitisha kifo cha Khamenei

Dismas Otuke
2 Min Read

Iran imethibitisha kifo cha kiongozi wake mkuu Ayatollah Ali Khamenei wa umri wa miaka 86, baada ya sintofahamu kuhusu hali yake kufuatia mashambulizi yaliyotekelezwa na Marekani nchini humo.

Tangazo kuhusu kifo cha Khamenei lilipeperushwa na runinga inayomilikiwa na serikali ya Iran mapema leo Jumapili.

Haya yanajiri saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kuuawa kwa Khamenei katika mashambulizi yao ya pamoja na Israel dhidi ya makazi ya Khamenei na sehemu nyingine jana Jumamosi.

“Tunatangazia watu wa Iran kwamba kiongozi mkuu Ayatollah Imam Sayyid Ali Khamenei, kiongozi wa mapinduzi ya kiisilamu, aliuawa katika mashambulizi ya Marekani Jumamosi Februari 28, 2026” lilisema tangazo la shirika hilo la habari la Tasnim.

Tangazo hilo lilielezea pia kwamba binti ya Khamenei, mkaza mwana na mjukuu nao waliuawa kwenye shambulizi hilo.

Awali Jumamosi, viongozi mbali mbali wa serikali ya Iran walikanusha habari za kifo cha Khamenei wakisema wanaamini yuko hai.

Khamenei aliingia uongozini nchini Iran mwaka 1989, baada ya kifo cha Ayatollah Ruhollah Khomeini, aliyeongoza mapinduzi ya waisilamu awali.

Khomeini aliongoza katika mawazo kwenye mapinduzi hayo yaliyokomesha uongozi wa ufalume wa Pahlavi huku Khamenei akihuisha mapinduzi hayo kwa kupanga jeshi.

Baada ya mashambulizi hayo, Rais Trump sasa anasema kwamba diplomasia ni rahisi katika kusuluhisha mizozo ikilinganishwa na mapigano.

Share This Article