Ukraine: Waafrika zaidi ya 1,700 wanapigana kwa niaba ya Urusi

Tom Mathinji
2 Min Read

Waafrika wapatao 1,700 wanashiriki kwenye vita kati ya Urusi na Ukraine.

Akitoa madai hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, alisema Moscow inatumia udanganyifu kuwashawishi raia wa Afrika kujiunga na mapigano hayo.

Akiwa ameandamana na mwenzake wa Ghana Samuel Okudzeto Ablakwa, Sybiha alisema mazungumzo yanaendelea na serikali mbalimbali barani Afrika ili kuzuia raia wao kuhadaiwa katika mipango hiyo.

“Kwa mujibu wa takwimu zetu, kwa sasa kuna zaidi ya raia 1,780 kutoka bara la Afrika wanaopigana katika jeshi la Urusi,” alisema Sybiha.

Aliongeza kuwa wapiganaji hao wanatoka katika nchi 36 tofauti za Afrika.

Hata hivyo, mamlaka za Urusi zimekanusha madai ya kuwaajiri kinyume cha sheria raia wa Afrika kujiunga na majeshi yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, alisema wengi wa Waafrika wanaopigana kwa niaba ya Urusi ni waathiriwa waliotapeliwa, wakihadaiwa kupitia mtandao wa siri (dark web) kwa ahadi za ajira za kawaida.

“Hawana historia ya kiusalama. Hawana uzoefu wa kijeshi. Hawajapata mafunzo,” alisema Ablakwa.

“Walishawishiwa na kudanganywa, kisha wakawekwa mstari wa mbele vitani.”

Ablakwa alionesha mshikamano wake na Ukraine na akatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili kumaliza vita hivyo, ambavyo vilitimiza miaka minne tangu kuanza kwake siku ya Jumanne.

Aidha, Ablakwa alisema Ghana itahamasisha kampeni za uelimishaji wa umma kuhusu mitandao ya usafirishaji haramu wa watu inayowadanganya Waafrika kujiunga na majeshi ya Urusi, wakati wa uongozi wake katika Umoja wa Afrika.

TAGGED:
Share This Article