Kesi ya Lissu yahamishiwa mahakama kuu

Kesi hiyo imekuwa ikiendelea katika mahakama ya hakimu mkuu mkazi ya Kisutu tangu Aprili.

Marion Bosire
2 Min Read
Kiongozi wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu

Kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA Tundu Lissu sasa imehamishiwa katika mahakama kuu.

Uamuzi huu ulitolewa na mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu katika kikao kilichoandaliwa jana Agosti 18, 2025 kati ya saa nne asubuhi na saa 11 jioni.

Kabla ya uamuzi huo kutolewa, Lissu alisomewa maelezo ya mashahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.

Mahakama hiyo pia ilikubaliana na uamuzi wa Agosti 4, 2025 wa mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam uliotolewa na jaji Hussein Matembwa.

Katika uamuzi huo, jaji Matembwa alielekeza kwamba maudhui ya mashahidi wa kiraia yasitolewe mubashara na hivyo kupiga marufuku vyombo vya habari kupeperusha moja kwa moja matukio ya kesi hiyo.

Hakimu Kiswaga alielezea kwamba shauri hilo sasa limekabidhiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria na mshtakiwa atapata taarifa ya mwenendo wa kesi hiyo kupitia Naibu Msajili wa Mahakama, ikiwemo tarehe atakayopangiwa.

Katika kesi hiyo Lissu anadaiwa kuchochea umma kutoshiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuandaliwa Oktoba 2025 kupitia matamshi aliyotoa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Lissu amekuwa kizuizini tangu alipokamatwa kwa mara ya kwanza Aprili 9, 2025 na anakabiliwa na mashtaka mengine ya kuchapisha habari zisizo za ukweli.

Makosa yake yote yanatokana na kampeni aliyokuwa akiongoza ya “No reforms No elections” iliyolenga kuchochea mabadiliko fulani kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa nchini Tanzania.

Share This Article