Watu sita wamefariki na wengine wawili kujeruhiwa baada ya ndege ndogo ya madaktari wa angani wa shirika la AMREF kuanguka katika eneo la makazi eneo la Mwihoko kaunti ya Kiambu Alhamisi alasiri.
Ndege hiyo kwa jina Cessna Citation XLS, iliyo na namba ya usajili 5Y-FDM, ilikuwa na abiria wanne ilipoanguka katika hali ambayo haikueleweka.
Akizungumza na wanahabari, kamishna wa kaunti ya Kiambu Henry Wafula alithibitisha hatua hiyo, akisema waliofariki ni madaktari wawili, wauguzi wawili na raia wawili waliokuwa ardhini. Alisema waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini.
Katika taarifa, mkurugenzi wa kitengo cha angani cha AMREF Stephen Gitau alisema ndege hiyo iliondoka uwanja wa ndege wa Wilson saa nane na dakika 17 alasiri ikielekea Hargeisa, Somalia, kabla ya kuanguka Mwihoko.
Aliongeza kwamba wanashirikiana kikamilifu na wadau wa uchukuzi wa angani na makundi ya misaada ya dharura kubaini hali halisi.