Rais wa Urusi, Vladimir Putin amependekeza mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine mjini Istanbul Mei 15, “bila masharti yoyote” ili kufanikisha “amani ya kudumu” na “kuondoa chanzo kikuu” cha mgogoro wa miaka mitatu.
Pendekezo hili lililotolewa mapema Jumapili, lilijiri saa chache baada ya viongozi wa Ukraine, Ufaransa, Ujerumani, Poland na Uingereza kutaka kusitishwa kwa mapigano kwa siku 30 kuanzia Jumatatu bila masharti.
Viongozi hao, waliokuwa wakikutana mjini Kyiv, walisema wito wao umeungwa mkono na Rais wa Marekani Donald Trump na walitishia kuiwekea Moscow vikwazo vipya “vikubwa” iwapo haitakubali mpango wao.
Putin hakujibu moja kwa moja wito huo katika kauli yake, lakini alikemea “vitisho” vya Ulaya na “matamshi ya chuki dhidi ya Urusi” kabla ya kueleza pendekezo la mazungumzo mapya kati ya Urusi na Ukraine.
“Tunapendekeza Kyiv irejee kwenye mazungumzo ya moja kwa moja bila masharti yoyote” alisema rais huyo wa Urusi kwa waandishi wa habari akiongeza kwamba hilo linafaa kufanyika Alhamisi hii mjini Istanbul.
Putin alisema atazungumza na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan baadaye Jumapili kusaidia kuratibu mazungumzo hayo.
Ukraine haikujibu mara moja kuhusu pendekezo hilo la Russia.
Hata hivyo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy awali alisema yuko tayari kwa mazungumzo ya amani, lakini baada ya kusitishwa kwa mapigano.
Uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine ulioanza Februari 2022 umesababisha vifo vya wanajeshi wengi na kuchochea mzozo mkubwa zaidi kati ya Urusi na Magharibi tangu Mgogoro wa Kombora la Cuba mwaka 1962.
Wajumbe wa Urusi na Ukraine waliwahi kufanya mazungumzo ya moja kwa moja mjini Istanbul katika wiki za mwanzo za mgogoro huo, lakini walishindwa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.