Rais Yoweri Museveni ametangazwa mshindi kwenye uchagzuzi wa Urais ulioandaliwa siku ya Alhamisi baada ya kupata asilimia 71.65 ya kura zote zilizopigwa.
Kulingana na Tume ya uchaguzi nchini Uganda, Museveni alipata kura 7,946,772 huku mpinzani wake wa karibu Robert Kyakulanyi almaarufu Bobi Wine akipata ku ra 2,741,238 sawia na asilimia 24.72.
Ikitangaza matokeo hayo Jumamosi jioni, tume hiyo ilisema kura 11,366,201 zilipigwa kwenye uchaguzi huo, ikiashiria asilimia 52.50 ya wapiga kura walioshiriki.
Museveni sasa ataongeza muda wake wa miaka 40 madarakani kwa miaka mitano zaidi.
Wakati huo huo Wine amepinga matokeo hayo na kuyataja ya ulaghai, huku akiwataka raia wa nchi hiyo kushiriki maandamano ya amani.
Aidha ametaka kurejeshwa mara moja kwa huduma za mtandao nchini humo.
Mamlaka nchini humo yalisema hatua ya kusitisha huduma za mtandao ilikuwa muhimu ili kuzuia uenezaji wa taarifa potovu, ulaghai wa uchaguzi na uchochezi wa ghasia.
