Viongozi Kitui wakemea mashambulizi dhidi ya MCA

Marion Bosire
1 Min Read
Kelvin Kinengo Katisya, Spika, Bunge la Kaunti ya Kitui

Viongozi wa Bunge la Kaunti ya Kitui, wakiongozwa na Spika Kelvin Kinengo Katisya, wamekemea vikali tukio ambalo mwakilishi wadi alivamiwa. 

Hayo yalitokea Jumamosi wakati wa mazishi katika eneo la Nuu, Kaunti Ndogo ya Mwingi ya Kati.

Akizungumza na wanahabari katika majengo ya Bunge la Kaunti ya Kitui, Spika Kinengo alilaani tukio hilo akisema waliohusika lazima wachukuliwe hatua za kisheria.

Aliwataka viongozi kudumisha amani na mshikamano wanapohudhuria mikutano ya hadhara.

Spika huyo pia aliwahimiza vijana kutojiingiza katika vitendo vya vurugu kwa kushawishiwa na wanasiasa kwa maslahi binafsi.

Aliwataka vijana kujitenga na matumizi mabaya ya kisiasa na kuendeleza amani katika jamii.

Mwakilishi wa wadi ya Nguni Jeremiah Musee Mutua anaripotiwa kuvamiwa Jumamosi iliyopita na kundi la vijana linalodaiwa kuhamasishwa na mfanyakazi mmoja wa serikali ya kaunti ya Kitui.

Tatizo kulingana na Spika Katisya lilitokana na hatua ya mwakilishi wadi huyo ya kuwa kinyume na jambo alilokuwa amesema mfanyakazi husika wa serikali ya kaunti ya Kitui.

Katisya aliongeza kusema kwamba mheshimiwa Mutua aliumia wakati wa tukio hilo kiasi cha kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Spika huyo alimalizia kuhimiza viongozi kukoma kupiga siasa za fujo na wavumiliane wanapotofautiana katika maoni.

Website |  + posts
Share This Article