Silaha haramu yapatikana huko Mutuati, kaunti ya Meru

Mshukiwa aliyetambuliwa kama Joyson Muchoki alikamatwa na maafisa wa usalama.

Marion Bosire
2 Min Read

Maafisa wa usalama katika kaunti ndogo ya Mutuati, kaunti ya Meru, wamemkamata mshukiwa mmoja na kupata bunduki moja haramu na risasi sita kutoka kwake.

Kulingana na Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Mutuati, Joel Kieti, mshukiwa aliyetambuliwa kama Joyson Muchoki ni mshukiwa wa mauaji aliyewahi kuhukumiwa awali.

Alikamatwa baada ya maafisa wa usalama kufanya msako uliodumu miezi mitano. Inadaiwa kuwa mshukiwa aliwatishia ndugu zake na machifu wa eneo hilo akidai kwamba angewapiga risasi.

Kieti alisema mshukiwa alikuwa mmoja wa wanachama wa genge la wahalifu ambalo limekuwa likitishia wakazi wa eneo hilo.

Alibainisha kuwa mwaka jana, maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI katika kaunti hiyo ndogo walipata bunduki zingine mbili haramu.

Aliongeza kuwa mshukiwa alikamatwa baada ya wanajamii kutoa taarifa muhimu kwa maafisa wa usalama kuhusu mahali alikuwa.

Chifu wa eneo la Naathu katika kaunti ndogo ya Mutuati, Charles Ntiriki, aliwashukuru wanajamii kwa kujitolea kutoa taarifa zilizosaidia kukamatwa kwa mshukiwa huyo.

Aliwahimiza wakazi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Matukio ya ukosefu wa usalama katika eneo la Mutuati yamekuwa yakiongezeka katika miezi ya hivi karibuni, huku waendesha bodaboda wakiwa miongoni mwa waathiriwa wakuu kwani wahalifu wenye silaha huwalenga ili kuiba pikipiki zao.

Share This Article