Saif al-Islam Gadaffi mwana wa Rais wa zamani wa Libya ameuawa

BBC
By
BBC
2 Min Read
Saif al-Islam Gaddafi, ameripotiwa kuuawa nchini Libya. Picha/Hisani.

Mwana wa kiume wa aliyekuwa Rais wa Libya Kanali Muammar Gaddafi, Saif al-Islam Gadaffi ameuawa nyumbani kwake katika jiji la Zintan.

Kifo cha mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 53, ambaye hapo awali alionekana kuwa mrithi wa baba yake, kilithibitishwa na mkuu wa timu yake ya kisiasa siku ya Jumanne, kulingana na Shirika la habari la Libya.

Hata hivyo, dada yake alitoa taarifa zinazokinzana na hizo akiambia televisheni ya Libya kwamba alifariki karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

Saif al-Islam Gaddafi kwa muda mrefu alionekana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa na anayeogopwa zaidi nchini baada ya baba yake, ambaye alitawala Libya kuanzia 1969 hadi alipoondolewa madarakani na kuuawa wakati wa uasi mwaka 2011.

Alizaliwa mwaka wa 1972 na kuchukua jukumu muhimu katika uhusiano wa Libya na nchi za Magharibi kuanzia mwaka wa 2000 hadi kuanguka kwa utawala wa Gaddafi.

Baada ya kuondolewa kwa baba yake, Saif al-Islam Gaddafi – ambaye alishutumiwa kwa kuchukua jukumu muhimu katika ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya kupinga serikali – alifungwa jela na wanamgambo wapinzani katika jiji la Zintan kwa karibu miaka sita.

>Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitaka kumshtaki kwa uhalifu dhidi ya binadamu kwa madai ya jukumu lake katika kukandamiza maandamano ya upinzani mwaka wa 2011.

Mnamo mwaka wa 2015, alipewa hukumu ya kifo bila kuwepo mahakamani na mahakama ya Libya kwa jukumu lake katika msako huo.

Gaddafi alikuwa akikana kila mara kwamba alitaka kurithi madaraka kutoka kwa baba yake, akisema hatamu za madaraka hazikuwa “shamba la kurithi”.

Hata hivyo, mwaka wa 2021 alitangaza kwamba angegombea urais katika chaguzi ambazo baadaye ziliahirishwa kwa muda usiojulikana.

BBC
+ posts
Share This Article