Rose Muhando afunguka kuhusu kunyanyaswa

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili nchini Tanzania, Rose Muhando, amefunguka kuhusu kile anachokitaja kuwa kudhulumiwa.

Muhando anadai kukoseshwa haki zake za mapato ya kazi zake za muziki baada ya kunyamaza kwa takribani miaka 15.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Rose amesema maumivu aliyoyavumilia kwa muda mrefu yamemlazimisha kuzungumza na kusema ukweli kuhusu kilichokuwa kikimkabili kimyakimya.

Rose Muhando ameeleza kuwa kwa kipindi chote hicho amekuwa akinyimwa haki yake ya mapato yatokanayo na kazi zake zilizopo kwenye majukwaa mbalimbali ya kidijitali.

Ameeleza kuwa hali hiyo inatokana na ushirikiano wake wa zamani na kampuni ya Sony Music Africa, ambayo licha ya ushirikiano huo kuvunjika kitambo, bado inashikilia zaidi ya kazi zake 37 na kukataa kuziachia.

Kwa mujibu wa msanii huyo, hajawahi kupata hata shilingi moja kutokana na kazi hizo, hali anayorejelea kama dhuluma kubwa dhidi ya jasho la maisha yake.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia afisi ya hakimiliki COSOTA, imejaribu kumsaidia kudai haki yake, lakini juhudi hizo zimekwama kutokana na kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa mwakilishi wa kampuni hiyo.

Rose ambaye alichapisha barua ya mwaka jana kutoka kwa COSOTA kwa kampuni ya Sony, amesema hali hiyo imemvunja moyo na kurudisha nyuma ndoto za wasanii wengi wanaodhulumiwa haki zao kimyakimya.

Kwa unyenyekevu, Rose Muhando ameiomba Serikali kupitia Waziri Paul Christian Makonda kuingilia kati suala hilo haraka ili haki itendeke, jasho la msanii liheshimiwe, na ndoto za wasanii zisizidi kukandamizwa.

Website |  + posts
Share This Article