Ray J ashtua mashabiki na taarifa kuhusu afya yake

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa mtindo wa R&B nchini Marekani Ray J, ameshtua mashabiki wake na taarifa ya kuhuzunisha kuhusu hali yake ya kiafya.

Haya yanajiri baada ya mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni William Ray Norwood Jr, kulazwa hospitalini akiugua ugonjwa wa pneumonia na maumivu kwenye moyo.

Akizungumza wakati wa mtagusano mubashara na mashabiki kwenye Instagram, msanii huyo alifuchua kwamba huenda akaaga dunia hivi karibuni.

Alielezea kwamba madaktari walimfahamisha kwamba moyo wake unafanya kazi kwa kiwango cha asilimia 25 pekee, akiongeza kusema kwamba hali yake ilibadilika ghafla.

Ray J wa umri wa miaka 45 alilazwa katika hospitali ya Las Vegas mwanzo wa mwezi huu na anaamini kwamba mwaka 2027 ndio mwisho wake.

J pia ameweka wazi jinsi miaka ya matumizi makubwa ya pombe na dawa za kulevya ikiwemo Adderall na nyingine zilivyomuumiza moyo wake.

Alifafanua kwamba sehemu ya moyo wake imeharibika vibaya na alisema kuwa awali alidhani mwili wake ungeweza kustahimili athari za mtindo wake wa maisha.

Msanii huyo alijilaumu kwa kuendeleza mtindo mbaya wa maisha akidhania kwamba mwili wake ungehimili athari za pombe na dawa za kulevya.

Ray ambaye ana mtoto wa kike aitwaye Melody wa miaka 7 na wa kiume aitwaye Epik wa miaka 5 na mpenzi wake wa awali Princess Love alishukuru mashabiki kwa kumuunga mkono.

Website |  + posts
Share This Article