Rais Ruto apeleka mpango wa Nyota Kaskazini mwa Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto leo amezindua utoaji wa shilingi milioni 103.9 chini ya mpango wa NYOTA wa mtaji wa kuanzisha biashara, unaolenga kuwezesha vijana kuendesha biashara katika kaunti za Samburu, Isiolo, Laikipia na Marsabit.

Mpango huu utanufaisha wajasiriamali vijana wapatao 4,159 kutoka kaunti hizo nne, ambapo kila mmoja atapokea shilingi 25,000 kwa ajili ya kuanzisha biashara mpya au kupanua zilizopo.

Mpango huo ni sehemu ya ajenda pana ya serikali ya kukuza ajira kwa vijana, maendeleo ya ujasiriamali na ujumuishaji wa kifedha.

Kwa mujibu wa mfumo wa utoaji wa fedha, shilingi elfu 22, zitawekwa moja kwa moja katika akaunti za Pochi La Biashara ili kusaidia shughuli za kila siku za biashara.

Shilingi elfu 3 zilizobaki zitawekwa kama akiba katika hazina ya taifa ya hifadhi ya jamii – NSSF, kwa lengo la kuhimiza utamaduni wa kuweka akiba miongoni mwa wajasiriamali vijana.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika eneo la Archers Post, Rais Ruto alisisitiza dhamira ya serikali ya kuwaunga mkono vijana kama nguzo muhimu za ukuaji wa uchumi, hususan katika maeneo ambayo hayajahudumiwa vya kutosha.

Alibainisha kuwa uwekezaji makhsusi kama Mpango wa NYOTA unalenga kufungua fursa za kiuchumi za maeneo ya ndani, kuimarisha biashara ndogo na kuunda ajira endelevu.

Mpango wa NYOTA unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi katika ngazi ya jamii na kuongeza ustahimilivu wa biashara zinazomilikiwa na vijana kaskazini mwa Kenya.

Website |  + posts
Share This Article