Omollo asifia mafanikio ya amani Mogotio na Kerio

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu wa usalama wa Taifa Raymond Omollo, amesifia mafanikio makubwa ya amani yaliyopatikana katika eneo la Mogotio na Bonde la Kerio kwa jumla.

Omollo amelilitaka Kanisa kushirikiana na Serikali katika kulinda uthabiti na kuimarisha maadili mema ya jamii.

Akizungumza katika ibada ya Kanisa la Waadventista wa Sabato huko Mogotio, Omollo alisema kuwa operesheni endelevu za kiusalama dhidi ya ujangili na wizi wa mifugo zinaonyesha matokeo chanya.

Kulingana naye oparesheni hizo zimeunda mazingira bora ya maendeleo, akihimiza wakazi, wazee wa jamii na viongozi wa dini kusaidia kudumisha mafanikio hayo.

Katibu huyo alionya wahalifu wanaolenga vijana kupitia dawa za kulevya na vitendo vingine haramu kwamba Serikali itachukua hatua kali, akisisitiza kuwa kulinda watoto na vijana ni kipaumbele kisichoweza kujadiliwa.

Kuhusu utoaji wa huduma Omollo alitangaza kuanza kwa utekelezaji wa vitengo vipya vya kiutawala vilivyotangazwa rasmi ili kusogeza huduma za Serikali karibu zaidi na wananchi.

Mogotio pekee imepata maeneo mapya matatu na kata ndogo tatu, huku katika Kaunti ya Baringo Serikali ikitarajia kuanzisha divisheni tano, zaidi ya maeneo 20 na zaidi ya kata ndogo 40.

Katika hotuba yake, Omollo alikumbusha waumini kuhusu agizo la Rais William Ruto kwamba hakuna mtoto anayepaswa kukosa masomo kwa sababu ya ukosefu wa karo, sare au viatu.

Alibainisha kuwa kiwango cha mpito cha Kaunti ya Baringo kwa sasa kimesimama kwa asilimia 71, huku juhudi zikiendelea kufikia asilimia 100.

Omollo pia aliangazia mipango ya kuwezesha vijana, kama mpango wa NYOTA, ambapo vijana 70 katika kila wadi watapokea ruzuku ya shilingi 50,000.

Alisema serikali pia inatekeleza mipango ya kutambua na kuthibitisha ujuzi unaoweza kufungua fursa za ajira nchini na nje ya nchi.

Alitaja miradi ya nyumba za gharama nafuu, masoko na miradi mingine Mogotio kama ushahidi wa ajenda jumuishi ya maendeleo ya Serikali.

Mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek, alihimiza wakazi, hususan vijana, kujisajili kupata vitambulisho vya taifa na kushiriki kikamilifu katika masuala ya uraia, akisisitiza uhusiano kati ya amani, maendeleo na uwajibikaji wa raia.

Website |  + posts
Share This Article