Mwanamuziki wa nyimbo za injili Ron Kenoly ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 81.
Kifo cha Kenoly kilichotokea Februari 3,2026, kilitangazwa na mkurugenzi wake wa muziki wa muda mrefu Bruno Miranda.
“Kwa zaidi ya muda wa miaka 20, nimekuwa na fursa ya kufanyakazi naye kote ulimwenguni, sio tu kama mkurugenzi wake wa muziki, lakini pia kama mwana wake, mwanafunzi na aliyeshuhudia maisha yaliyojaa uaminifu,” alisema Miranda.
Ron aliyezaliwa nchini Marekani, pia alihudumu kwa jeshi la nchi hiyo kati ya mwaka 1965 na 1968 chini ya bendi iliyofahamika Mellow Fellows.
Baada ya kuhudumu kwa jeshi, Kenoly alirejea Los Angeles na kujitosa kikamilifu kwa muziki, safari iliyomfanya kuwa kiongozi mashuhuri wa nyimbo za injili katika kizazi chake.
Huku chanzo cha kifo chake kikikosa kubainishwa, Kenoly amemwacha mke wake Tavita, na watoto wake watatu Samuel, Ronald, na Tony.
