Msichana ajitoa uhai Narok kwa kutoridhika na matokeo ya KCSE

Kisa hicho kilitokea jana jioni, muda mfupi baada ya matokeo ya KCSE kutangazwa.

Marion Bosire
1 Min Read

Msichana mmoja anaripotiwa kujitoa uhai katika kijiji cha Manyatta, Lokesheni ya Sossiana kaunti ya Narok kufuatia kutoridhika na majibu yake ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE.

Kulingana na taarifa ya maafisa wa polisi wa kituo kidogo cha Esoit, msichana huyo kwa jina Missipah Chepkurui alifahamu matokeo yake ya alama ya C jana Januari 9, 2025, kupitia kwa simu ya babake aitwaye Josiah Koech.

Hakuamini matokeo hayo lakini baba akamfahamisha kwamba alikuwa ameyahakiki kupitia kwa simu ya mjomba wake na akaonekana asiye na furaha.

Binti huyo wa umri wa miaka 20 hakusema na yeyote nyumbani humo hadi jioni wakati mamake kwa jina Mirriam koech alisikika akipiga mayowe.

Waliofika walipata kwamba Missipah alikuwa mnyonge baada ya kubugia kemikali isiyojulikana akijaribu kujitoa uhai.

Walimkimbiza hospitali ya Kurangurik level 3 wakapatiwa rufaa hadi hospitali ya Danai level 4 kwa matibabu zaidi na alipofikishwa huko akadhibitishwa kwamba amefariki.

Mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya kilgoris level 4 kusubiri uchunguzi zaidi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *