Watu zaidi ya 2,000 wameuawa wakati wa msako mkali wa vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji nchini Iran, kundi la haki za binadamu limesema, huku Rais Trump akiwaahidi Wairani kwamba msaada “unakaribia”.
Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake nchini Marekani (HRANA), liliripoti kwamba hadi sasa limethibitisha mauaji ya waandamanaji 1,850, watu 135 walioshirikiana na serikali, raia wengine tisa pamoja na watoto tisa katika kipindi cha siku 17 zilizopita licha ya kukatika kwa mtandao.
Afisa mmoja wa Iran pia aliambia shirika la habari la Reuters kwamba watu 2,000 wameuawa lakini “magaidi” ndio wa kulaumiwa.
Trump atahudhuria mkutano kuhusu Iran Jumanne jioni, na ameahidi kupata takwimu “sahihi” za vifo.
“Idadi ya waliouawa inaonekana kuwa kubwa lakini bado hatuna taarifa za uhakika,” Trump aliwaambia waandishi wa habari wakati akirejea Ikulu ya White House.
Mara tu atakapopata idadi kamili, alisema, “tutachukua hatua ipasavyo.”
Mapema Jumanne, Trump aliandika kwenye jukwaa lake la Truth Social kwamba mamlaka ya Iran “italipa gharama kubwa” kwa mauaji hayo, na akawasihi watu “waendelee kuandamana”.