Jeshi limehimizwa likumbatie teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuimarisha shughuli zake na kuhifadhi urithi wa kitamaduni.
Wito huo ulitolewa wakati wa maadhimisho ya siku ya utamaduni ya Jeshi la Ulinzi la Kenya – KDF yaliyofanyika jana Jumamosi katika bustani ya Uhuru, jijini Nairobi.
Hafla hiyo ya kupendeza iliwakutanisha wanajeshi, familia zao, wanadiplomasia na raia na kuonyesha kwa njia ya kuvutia tamaduni mbalimbali za Kenya pamoja na mila kutoka zaidi ya mataifa 22 washirika.
Maadhimisho ya mwaka huu yalifanyika chini ya kaulimbiu Utamaduni na Teknolojia, yakisisitiza nafasi inayoongezeka ya ubunifu katika kulinda urithi wa kitamaduni kwa vizazi vijavyo.
Waziri wa Ulinzi, Soipan Tuya, aliwataka maafisa wa jeshi kutumia teknolojia ya kisasa sio tu kuboresha ufanisi wa kiutendaji, bali pia kurekodi, kuhifadhi na kukuza utambulisho wa kitamaduni ndani ya jeshi.
Alibainisha kuwa ubunifu unatoa fursa mpya za kulinda mila huku ukisaidia kukabiliana na mabadiliko ya haraka ya dunia ya sasa.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Charles Kahariri, aliunga mkono kauli hiyo akisisitiza kuwa teknolojia ni muhimu katika kulinda urithi wa kitamaduni.
Aliongeza kusema kwamba teknolojia ni muhimu katika kuimarisha umoja na kukuza mshikamano na kuishi kwa amani miongoni mwa mataifa.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa kutambuliwa upya kwa utamaduni kama nguvu inayounganisha, kuimarisha huduma ya kijeshi, kukuza mshikamano na kujenga mahusiano baina ya mataifa kuvuka mipaka.
