Israel imesema itafungua kwa muda, mpaka wa Rafah wa Gaza na Misri mara tu operesheni ya kutafuta mwili wa mateka wa mwisho wa Israel aliyebaki katika eneo la Palestina itakapokamilika.
Tangazo hilo kutoka kwa afisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, lilitolewa jana Jumapili jioni, wakati Wapalestina walikuwa wakiomboleza angalau watu watatu waliouawa katika mashambulizi ya Israel kote Gaza.
Afisi ya Netanyahu ilisema kuwa mpaka wa Rafah, ambao ulipaswa kufunguliwa katika awamu ya awali ya mpango wa kusitisha mapigano uliopatanishwa na Marekani mwezi Oktoba, utafunguliwa tena kwa ajili ya kupitisha watu pekee.
Ilisema hatua hiyo inategemea kurejeshwa kwa mateka wote walio hai na utekelezaji wa juhudi kwa asilimia 100 kwa upande wa Hamas za kuwapata na kuwarejesha mateka wote waliokufa.
Wote wamerejeshwa, isipokuwa mwili wa afisa wa polisi Ran Gvili.
Jeshi la Israel lilisema Jumapili kuwa lilikuwa likichunguza makaburi kaskazini mwa Gaza karibu na mstari wa njano unaotenganisha maeneo yanayodhibitiwa na Israel.
Afisa mmoja wa jeshi la Israel alisema kulikuwa na vidokezo kadhaa vya kijasusi kuhusu mahali anapoweza kuwa Gvili.
Mapema Jumapili, Hamas ilisema kuwa ilikuwa imetoa kwa uwazi habari kuhusu eneo ambapo mabaki ya askari huyo wa Israel yanaweza kupatikana.
Hamas ilisema pia kwamba imetimiza wajibu wake wote kulingana na makubaliano ya kusitisha mapigano.
Msemaji wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za Qassam, alisema kundi hilo limejitolea kikamilifu kufunga suala hili kabisa na halina nia ya kuchelewesha.
