IPOA yaanzisha uchunguzi dhidi ya ukatili wa polisi Nandi

Tom Mathinji
1 Min Read
Issack Hassan - Mwenyekiti wa IPOA

Halmashauri Huru ya kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA) imelaani vikali kisa ambapo maafisa wa polisi waliwavamia na kuwachapa vijana waliokuwa wakicheza mchezo wa pool katika kaunti ya Nandi.

Kupitia kwa taarifa Ijumaa jioni iliyotiwa saini na mwenyekiti wa IPOA Ahmed Issack Hassan, halmashauri hiyo ilisema imewapeleka maafisa wake kuchunguza kwa kina swala hilo, kutathmini mienendo ya maafisa wa polisi waliohusika na kubainisha hatia zao.

IPOA ilitaja kitendo hicho kuwa ukiukaji wa kanuni za utendakazi wa polisi na katiba,na kutoa wito kwa waathiriwa kuwa watulivu huku uchunguzi ukiendelea.

Huduma ya Taifa ya Polisi pia imeshtumu kisa hicho, huku hatibu wa polisi Muchiri Nyaga akidokeza kuwa kuwa mienendo ya maafisa hao ilikuwa ukiukaji wa sheria inayosimamia huduma ya taifa ya polisi,kanuni za maadili ya polisi na haki msingi za binadamu,akiongeza kuwa uchunguzi umeanza.

Kwenye kanda ya videoe iliyosambazwa mitandaoni,maafisa hao walivalia sare rasmi walionekana wakiingia ukumbi wa kucheza Pool mjini Nandi Hills na kuwaamrisha vijana hao kulala sakafuni na kisha kuanza kuwapiga,kabla ya kuondoka ukumbuni humo dakika nane badaye.

kwa upande wake Gavana wa Nandi Stephen Sang ameshtumu kisa hicho akitoa wito wa uchunguzi wa kina kuhakikisha hatua kali za kinidhamu zinachukuliwa dhidi ya maafisa waliohusika.

Website |  + posts
Share This Article